16/10/2026
MKUU WA WILAYA YA MTWARA NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WATEMBELEA MAGHALA YA KISASA YA NHC
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Abdallah Mwaipaya, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amefanya ziara ya kutembelea maghala ya kisasa ya kuhifadhia nafaka na mazao mbalimbali yaliyojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Mtwara.
Katika ziara hiyo, Bw. Mwaipaya na ujumbe wake wamepokelewa na Meneja wa NHC Mkoa wa Mtwara, Bw. Joseph John Mwabusila, ambaye amewapatia maelezo kuhusu mradi huo na mchango wake katika kuboresha huduma za uhifadhi wa mazao na kuimarisha shughuli za biashara mkoani humo.
Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.146, umehusisha ujenzi wa maghala matatu ya kisasa katika awamu ya kwanza, kila moja likiwa na ukubwa wa mita za mraba 1,000. Maghala hayo yamekamilika na kukabidhiwa kwa ajili ya matumizi.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao, hususan korosho na nafaka, huku ukifungua fursa zaidi kwa wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji katika Mkoa wa Mtwara na maeneo jirani.
Kupitia mradi huu, NHC inaendelea kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara kwa kujenga miundombinu inayoongeza thamani ya mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi.