MWL. CHUSI

MWL. CHUSI Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Mithali 1:7

08/05/2023

SOMO: MUNGU HUJIFUNUA KATIKA KIWANGO HICHO HICHO UNACHOMJUA.๐Ÿ‡น๐Ÿ‡ฟ๐Ÿ‡ฎ๐Ÿ‡ฑ

Nakusalimu katika Jina Yesu Kristo, ndugu yangu katika Kristo Yesu.โœ๏ธ

SALA;
Neema na iwe kwenu ninyi nyote ndugu zangu katika Kristo Yesu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo, na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema Mungu wa faraja yote.
Amina ๐Ÿ™๐Ÿ™๐Ÿ™

UTANGULIZI:

Sikia mpendwa kiwango chako cha kumjua Mungu ndio mpaka wako wa ufahamu juu ya Mungu.

Kiwango chako cha ufahamu juu Mungu ndicho kiwango cha imani uliyonayo. Hakika haiwezi kwenda mbali ya ufahamu katika imani yako.

Kwa namna unavyokuwa karibu sana na Mungu ndivyo unavyomjua zaidi Mungu, alivyo mkuu na wa kuogofya sana. K**a vile ukiwa unaiona ndege/ Meri kwa ukaribu bila shaka unajua ilivyokubwa, ndivyo Mungu alivyo;

Isaya naye kwa kuwa hakuwa karibu sana na Mungu hapo awali, alimuona Mungu wa kawaida sana.
Lakini anasema โ€œ katika mwaka ule aliyokufa mfalme Uzia nalimuona Bwana ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekaluโ€. 5 Ndipo niliposema, Ole wangu kwa maana nimepotea;

Isaya 6:1-3
[1]Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

[2]Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.

[3]Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.

Isaya 6:4-5
[4]Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.

[5]Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi...๐Ÿ–Š

Ufafanuzi;
Haya yote anayasema nabii Isaya kwa sababu amemkaribia Mungu na kuona UKUU wake, naye anaogopa, kwa nini anaogopa anajiona yeye ni mchafu hastahiri kumtazama Mungu ndio maana anakiri uovu wake akisema, Mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona mfalme.

Lakini pia kumbe, kuna watu ukiwa nao karibu hautakuwa na ufahamu mkubwa juu ya Mungu, Nabii Isaya anasema; katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimuona Bwana.

Lakini pia nabii Habakuki, mwanzo alikuwa akilalamika za juu ya Mungu na kuona mbona hatendi vile alivyotaka yeye, lakini baada tu ya kumjua Mungu,amebadilika.
Anasema katika sara yake 2

โ€œEe Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopaโ€.


Lakini ukiwa mbali sana na Mungu ndivyo unavyo muona Mungu mdogo na hawezi kutatua shida zako.

Na wakristo wengi wako mahali hapa, ndio maana kunabaadhi ya wakristo wakipata shida kubwa hao hao wanakwenda kwa waganga wa kienyeji, Je! Ni kweli Mungu hawezi kutatua changamoto yako uliyonayo? Au umemuona Mungu mdogo na mganga mkubwa zaidi kuliko Mungu?

Ni kweli maisha yako yana vikwazo vingi uchumi ni mgumu Je! Umeona Mungu hawezi? Mpaka umeenda kwa miungu mingine? Nikwambie tu! Katika mambo ambayo ni chukizo sana mbele za Mungu ni kuomba msaada na kuabudu miungu mingine.

Ni kweli haujapata mchumba na umekuwa ukimngoja Bwana, mwishowe ukachoka na kwenda kutafuta msaada mahali pengine, je! Ni sawa?

Ni kweli unachangamoto ya ndoa lakini ndo uchukue maamuzi magumu na mabaya yenye kuthiri wengine, kweli utasema unamjua Mungu wewe!

Je! Ni kweli kuwa pombe ndio suruhisho la matatizo yako na stress ulizonazo, angalia vizuri mpendwa maana wakati mwingine mchawi wa maisha yako ni wewe mwenyewe.

Ni kweli una madeni sana, ndio uamue kujirahisi k**a wewe mama au binti kwa sababu ya pesa kweli unamjua na kumpenda Mungu wewe?

Unaweza ukamjua Mungu, kwa udogo, ukawaida au kwa ukubwa, itategemeana na vile Ufahamu ulionao juu ya Mungu.

Ni kweli hauna kazi sasa ndio udhurumu wengine na kuwa tapeli na kuiba,unadhani ni sawa!. Sikia mpendwa akipandacho mtu ndicho atakacho kivuna.

Ukipanda uzinzi utavuna magonjwa.
Ukipanda ulevi utavuna laana na uharibifu.
Ukipanda wizi utavuna laana na kutangatanga.
Ukipanda uzurulaji utavuna umasikini.
Maana mshahara (malipo) ya dhambi ni mauti.

Mpenzi katika kristo Yesu panda mbegu njema .

Ni kweli una uhitaji na hiyo kazi, sasa ndio utoe rushwa ili uipate hiyo kazi! Sasa utakuwa na utofauti gani kati yako wewe uliyeokoka na asiyeokokoka? Ikiwa nawe unaenenda k**a mataifa waenendavyo, Biblia inasema wala tusienende k**a mataifa.

Wapenzi katika kristo Yesu, tuache kumuahibisha kristo Yesu, kwa kuyafanya yasiyompendeza Mungu tunamfanya Yesu kana kwamba hakufanya chochote msalabani, ninaandika ujumbe huu nikiwa na uchungu sana na huku machozi yakinitiririka moyoni mwangu, maana katika kazi ambayo Bwana Mungu ameniitia ni kuwaambia watu juu ya nyakati za mwisho na amenipa kazi ya kuwalilia watu juu ya maovu yao...๐Ÿ–Š

Ushuhuda;
Siku moja nilikuwa katika maono ya usiku, nikachukuliwa na kupelekwa mahali fulani, nami nikaona bara bara Nzuri sana ya rami,

kisha nikaona watu wakipita na wote walikuwa wakielekea mwelekeo mmoja, na walikuwa wakielekea kusini, wengine walikuwa wakitembea kwa miguu na wengine walikuwa kwenye magari yao, na kati wa watu niliowaona niliwaona, mabinti wawili ambao ninawafahamu nilishawahi kuwaambia juu habari za Mungu.

Nao pia walikuwa katika safari hiyo na mikononi mwao walishika fimbo ambazo walizitembelea na walioneka k**a wazee sana na walitembea k**a wazee.

Nikauliza nini maana yake? Ndipo, Neno la Bwana likanijia kusema hii ndio njia walioichagua watu wengi sana, ambayo machoni inaonekana kuwa ni njema sana lakini kumbe ni njia za mauti.

Nilisikia hivi nikajikuta ninalia kilio kisicho cha kawaida, na wakati ninalia nilikuwa nikimwita binti mmoja kati ya wale ninaowafahamu, lakini alikuwa akigeuka na kunitazama halafu anaendelea na safari, nilimwita mara tatu, lakini haikusaidia.

Kulipokucha asubuhi, nilianza kutafakari maono hayo nikajikuta nina uchungu na ninalia tu moyoni,
ikaja mistari kutoka kitabu cha mithali 14:12 iliyosema masikioni mwangu kuwa โ€œ 12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, lakini mwisho wake ni njia za mautiโ€
Ni kwa sababu hauoni....๐Ÿ–Š

ZINGATIA MAHUSIA YA BWANA.

Mpendwa weka shauku ndani yako ya kumpenda Yesu naye ataonekana kwako.

kuna wakati tunampa Mungu wakati mgumu sana, hapendi tuangamie,

Maombolezo 3 32 โ€œMaana moyo wake (Mungu) haupendi kuwatesa wanadamu wala kuwahizunishaโ€

Kuna wakati Mungu anataka kutuangamiza kwa sababu ya dhambi lakini anaona wasiomjua Mungu na shetani watatucheka na kusema, tazama Mungu wao yuko wapi mbona amewatelekeza na kuwaacha katika uharibifu? Na uharibifu umewapata.

Na ndio maana Mungu alileta neema na kuachana na sheria kwa maana kwa sheria aliona hakuna mwadamu angeweza kustahiri na kuokoka kutoka katika dhambi, tazama kitabu cha;

Waebrania 10:16
[16]Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana,
Nitatia sheria zangu mioyoni mwao,
Na katika nia zao nitaziandika;
ndipo anenapo.

Mpendwa kuna saa inakuja wala si mbali bali karibu.

UJUMBE HUU NI KWA AJIRI YAKO MPENDWA.

Leo kwa neema na kibari cha Mungu napenda tujifunze namna Mungu anajifunua/ anadhirika kwenye maisha yetu.

Watu wengi hawafahamu siri hii, lakini ni ukweli usiopingika kuwa kiwango chako cha kumjua Mungu ndicho kiwango hicho hicho Bwana Mungu atajifunua kwako.

Je! Unamjua Bwana Mungu k**a nani?

Kwanza kabisa tambua ya kuwa;

Mungu ni Roho,
Yohana 4:24 Biblia inasema โ€œ Mungu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na kweliโ€

Ufafanuzi;
Na k**a Mungu ni Roho basi unapaswa kumjua Mungu katika namna ya kiroho na si namna ya kimwili.

Hivyo basi hata kumjua Mungu ni tendo la kiimani, maana Mungu ni Roho, Biblia inasema.

katika Waebrania 11 : 1-3 โ€œ Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. 2 Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. 3 Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu. Hata vitu visivyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.

Ufafanuzi;
sasa tunajifunza kuwa, kumbe kuwa na ufahamu wa kimungu inakuhitaji uwe na imani kwa maana haya ni mambo yasiyoonekana lakini ni bayana yaani yapo, na pia kumbe kuwa na imani kubwa kwa Mungu aliyezifanya mbingu na nchi inakuhitaji uwe na ufahamu wa kimungu na ufahamu unapatikana katika neno lake yaani Biblia takatifu.

Sasa kuna watu wana imani lakini wamekosa ufahamu wa kimungu na wengine wana ufahamu tu k**a mafarisayo lakini wamekosa imani kumbuka haya ni mambo ya kiroho kabisa.

Ndio maana neno la Mungu linasema mna macho lakini hamuoni na mna masikio lakini hamsikii, hii ina maana ya macho ya kiroho na masikio ya kiroho na sio haya ya nyama yaani ya mwili.

Ezekieli 12:1-2
โ€œ Neno la Bwana likanijia tena, kusema 2 Mwanadamu wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, lakini hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi.

Ufafanuzi;
Kumbe dhambi ina leta giza katika macho, masikio na ufahamu.

Sasa ili kukua kiroho na kumjua Mungu zaidi ya vile tunavyomjua, tunapaswa kuwa na imani pamoja na ufahamu wa kimungu.

Biblia inasema imani pasipo matendo imekufa, na mimi k**a mtumishi wa Mungu, ninasema kuwa imani pasipo ufahamu wa kimungu imekufa pia.

Hivyo basi;
Msingi wa kukua kiroho na kutembea na Mungu katika roho na kweli inakuhitaji kuwa na;





Vinakwenda sambamba, utasema unaamini nini ikiwa hauna ufahamu wa mambo hayo, watu wengi sana wamekwama hapa, wakiamini kuwa na imani na matendo inatosha kabisa lakini leo nataka nikwambie mtu wa Mungu, tafuta maarifa pia ili namna yako ya kumjua Mungu ikue.

Biblia inasema Hosea 4:6-7
โ€œwatu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi, kwa kuwa umesahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wakoโ€

Ukiwa una maarifa na ufahamu wa kimungu utakuwa huru.

โ€œIfahamu kweli nayo kweli itakuweka huruโ€

Ndio maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake akisema mngalikuwa na imani japo punje ya haradari (yaani japo kidogo) mngaliweza kuamuru mlima huu ngโ€™ooka nao ukatupwa baharini nao ungalitii,

Ufafanuzi;
Sasa hapo Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi wake juu ya โ€œNguvu ya imaniโ€ (The power of faith) lakini ndani yake kuna ufahamu wa kujua kuwa ndani yetu kuna nguvu ya kuamlisha vitu na vikawa, k**a vile Baba yetu Mungu alivyo na nguvu hii na sisi pia tunayo, Maana sisi ni warithi wake na ni wana wa agano, ila tatizo kubwa hatuna ufahamu.

Waefeso 3:20 โ€œ Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;โ€

Kumbe ndani Yetu kuna nguvu kubwa sana, lakini ni ngumu kuamini kwa sababu ya kukosa ufahamu.

Biblia inasema โ€œ kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa. Bali wapumbavu hudharau hekima na adabuโ€

Mpendwa jitathimini kiwango chako cha kumjua Mungu ndicho unachomwamini Mungu.

Kuna watu huwasema baadhi ya watumishi wa Mungu kwa miujiza inayofanyika wakitilia shaka (doubt) kuwa sio Mungu ni kweli wengine sio, maana Biblia inasema katika Ezekia 13:1-10 wako manabii ambao wamefanya ambayo Mungu hakuwatuma, kifupi wamesema uongo, na kutaniri uongo, hivyo basi ni manabii wa uongo.

Lakini wapo wakristo wengi ambao wanashaka na kila mtumishi, hususani manabii na mitume, wakiamini kabisa wanatumia nguvu za giza katika miujiza hiyo.

Si dhambi kuchunguza yupi ni mtumishi wa Mungu wa kweli, maana Biblia inasema zichunguzeni hizo roho.

Lakini jambo lingine la kujifunza ni kwamba watu wanashaka na Mungu kutokana tulivyomfahamu, au kukosa ufahamu wa kutosha juu ya Mungu. ukitia tu ufahamu juu ya Mungu imani yako inaongezeka papo hapo.

KUWA KIELELEZO BORA CHA KRISTO YESU.

ANGALIA UKRISTO WAKO USIWE KIKWAZO KWA WENGINE, WASIPATE KUMJUA MUNGU, MAANA SISI NI NURU YA ULIMWENGU HIVYO TUNAPASWA KUANGAZA NA WENGINE WAMJUE MUNGU BILA HATA KUWAAMBIA HABARI ZA MUNGU.
ILA KWA MATENDO YETU TU WAONE HAKIKA WATU HAWA WANAMWAKILISHA MUNGU WA MBINGUNI HAPA DUNIANI.

Kwa maana matendo yetu sisi wakristo yanamuhubiri Kristo zaidi kuliko hata kusema kwetu.

Ni maombi yangu kwa ajiri ya siku hii ya leo,
Mungu akupe ufahamu na umtazame Mungu kwa namna mpya.

MUNGU AKUBARIKI SANA.

By Mwl. Chusi Steven.
+255742874709
08/05/2023
Manyara - Tanzania
Stay Blessed.

SOMO: JIFUNZE NAMNA YA KUTEMBEA NA ROHO MTAKATIFU. ๐Ÿ“–  ๐Ÿ‡น๐Ÿ‡ฟ ๐Ÿ‡ฎ๐Ÿ‡ฑUTANGULIZI: Nakusalimu kwa jina la Yesu Kristo ndugu yangu ka...
05/05/2023

SOMO: JIFUNZE NAMNA YA KUTEMBEA NA ROHO MTAKATIFU. ๐Ÿ“– ๐Ÿ‡น๐Ÿ‡ฟ ๐Ÿ‡ฎ๐Ÿ‡ฑ

UTANGULIZI:
Nakusalimu kwa jina la Yesu Kristo ndugu yangu katika Kristo Yesu..โœ๏ธ

SALA;
Neema ya Bwana wetu Yesu kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae na sisi sote sasa na hata milele..
Amina.๐Ÿ™๐Ÿ™๐Ÿ™

MAANA YA ROHO MTAKATIFU.

Roho Mtakatifu ni nani?

Inawezekana ni swali ambalo umekuwa ukijiuliza kwa muda sasa na pengine haukupata majibu ya kukuridhisha, lakini siku ya leo Bwana Mungu amekusudia umuelewe vizuri, mjue sana Mungu ili uwe na amani, k**a kitabu cha Ayubu kinavyoeleza.

Ayubu 22:21
[21]Mjue sana Mungu, ili uwe na amani;
Ndivyo mema yatakavyokujia.

Nakusihi sana mtu wa Mungu fuatana pamoja na mimi, ili upate kuvuna maarifa haya ya ajabu.
Mithali 19:8
[8]Apataye hekima hujipenda nafsi yake;
Ashikaye ufahamu atapata mema.
Zaburi 139:6
[6]Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi,
Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.... ๐Ÿ–Š

MAANA YA ROHO MTAKATIFU.
Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu katika utatu Mtakatifu, yaani Baba, (Mungu) Mwana, (Yesu) na Roho Mtakatifu (Roho ya Mungu)

Mwanzo 1:26
[26]Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

Ufafanuzi;
Neno tumfanye mtu kwa mfano wetu na kwa sura yetu, inaashiria uwingi hivyo basi ni dhahiri kuwa, kulikuwa na Baba Mwana na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu, ni Roho ya Mungu na anakaa ndani ya Mungu baba, hivyo basi huwezi kumuona na macho ya damu na nyama, au kwa sura na umbo, kitabu cha Mwanzo 1:2 kinathibitisha kuwa Roho Mtakatifu ni Roho ya Mungu.

Mwanzo 1:2
[2]Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.

Lakini pia Chuo cha Isaya kinatuthibitishia kuwa Roho Mtakatifu ni Roho ya Mungu,
Isaya 61:1
[1]Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.

ZINGATIA:
Roho Mtakatifu sio kitu, sio maji, sio mwanga, sio hua au njiwa, sio moto, sio upepo k**a wengine wanavyodhani, badala yake hivyo ni namna Roho Mtakatifu anajifunua au kujidhihirisha katika maumbo mbali mbali, lakini haimaanishi kuwa ndio Roho Mtakatifu..

Roho Mtakatifu ni mtu kwa sababu ana sifa zote za kiutu, k**a ifuatavyo;

SIFA ZA KIUTU ZA ROHO MTAKATIFU;

i) Roho Mtakatifu ana hisia, yaani ana hisi hali, vitu na mambo, kwa sababu anaweza kuhisi hisia za huzuni au furaha, hususani pale tunapotenda dhambi Roho Mtakatifu huuzunika na kuugua ndani yetu k**a ishara ya kwamba hapendezwi na uovu, na ni hakika ya kwamba Mungu hachangamani na udhalimu.

Waefeso 4:30
[30]Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.

ii) Roho Mtakatifu ana wivu, yaani kumbe Roho Mtakatifu anasikia wivu! sasa utaniuliza ni wivu gani? Ni wivu wa kutaka ushirika na sisi wanadamu, sasa ikiwa sisi wanadamu tunampuuza au hatuutambui uwepo wake kwetu basi husikia wivu kwa maana anatutamani kiasi cha kuona wivu.

Yakobo 4:5
[5]Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? "

iii) Roho Mtakatifu ana akiri, ni kweli Roho Mtakatifu ana akiri ya ajabu sana, kwa maana yeye huyafumbua mafumbo yote ya Bwana Mungu na kuwafunulia wanadamu, yaani hata mimi kuna wakati mpaka namshangaa sana huyu Roho wa Mungu.

kwa maana nikiwa niko kufundisha Neno la Mungu, baasi huniletea mistari ya Biblia mfululizo mpaka nachanganyikiwa, na kila nitakachokisema ananikumbusha kwa kunipa mstari husika wa Biblia, hata k**a hauna kumbukumbu nzuri ila ukiongozwa na Roho Mtakatifu watu watakushangaa sana kuwa una akiri ya ajabu, lakini kumbe ni Roho Mtakatifu, hakika napenda sana kuongozwa na Roho wa Mungu, hebu tutazame katika kitabu cha 1Wakoritho kinatuthibitishia kuwa Roho Mtakatifu ana akiri tena ya ajabu sana..

1 Wakorintho 2:10-11
[10]Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.
[11]Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.

iv) Roho Mtakatifu ana nia au maamuzi, anaweza kuamua katika utendaji wake, kufanya mambo mbali mbali sawa sawa na mapenzi ya Mungu......
Kwa mfano; pale ambapo wanadamu hatuwezi yeye Roho Mtakatifu huchukua jukumu la kutusaidia, na kitendo hicho ni maamuzi ya kutusaidia, tazama katika kitabu cha Warumi..

Warumi 8:26
[26]Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

SIFA TATU MUHIMU ZA KIUTENDAJI ZA ROHO MTAKATIFU.

a) Sifa ya kwanza, Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu ni msaidizi, Yohana 14:16
[16]Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
sisi wanadamu tunahitaji sana msaada wa Roho Mtakatifu, k**a ambavyo unajua si rahisi sana kushinda dhambi na kuishi mapenzi ya Mungu, pamoja na kuyaishi maisha matakatifu na kuwa kielelezo cha Kristo Yesu, unajua kuna wakati unajikuta kuna dhambi fulani! Kila ukijaribu kuishinda na kujinasua katika uovu huo bado hauwezi, hata Paulo anazungumza juu ya ugumu ya jambo hili; ninamnukuu akisema katika kitabu cha;

Warumi 7:15-19
[15]Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.

[16]Lakini k**a nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.

[17]Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

[18]Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.

[19]Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.

Bwana Yesu asifiwe mtu wa Mungu, inawezekana hata wewe kuna dhambi umejaribu kuiacha kwa jitihada zako lakini hauwezi, na ni kweli hautaweza!, mwingine amejaribu kuacha uzinzi, mwingine kusengenya watu wengine, mwingine chuki, mwingine pombe, lakini hawezi kabisa tena anasema mimi sipendi hii hali lakini siwezi kuacha, leo nataka nikwambie ya kuwa Roho Mtakatifu ndiye dawa ya mambo yote, yasiyowezekana kwa wanadamu kwake Mungu yanawezekana..๐Ÿ–Š

b) Sifa ya pili ya Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu ni mwalimu, Yohana 14:26
[26]Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

Roho Mtakatifu ni mwalimu wa kweli kwa maana yale yote ambayo hatuyajui, basi yeye hutufundisha, kwa mfano ni ngumu sana kusoma na kuelewa neno la Mungu (Biblia) bila ufunuo wa Roho Mtakatifu, hivyo basi kitendo cha kukufunulia ndio kukufundisha, kuna wengine wameenda mbali zaidi katika mahusiano yao na Roho Mtakatifu, kwani hufundishwa katika ndoto na kupewa mafunuo na maarifa ya kimungu, nikwambie tu mpendwa ya kuwa hakuna raha k**a kutembea na Roho Mtakatifu.๐Ÿ–Š

c) Sifa ya tatu ya Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu ni kiongozi, Yohana 16:13
[13]Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Unajua taangu Bustani ya Edeni mwanadamu alipoteza uaminifu mbele za Mungu, baada ya kuasi na kutenda dhambi, hivyo basi Bwana Mungu hakumuacha tena mwanadamu ajiongoze mwenyewe, kwa sababu mwanadamu huyu hatamudu kuishi maisha matakatifu bila uongozi wa Roho Mtakatifu, ndio maana Yesu anawaambia wanafunzi wake ya kuwa hawawezi neno lolote pasipo yeye (Yesu) katika kile kitabu cha
Yohana 15:5
[5]Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.๐Ÿ–Š

Yohana 14:18
[18]Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.
[16]Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
[17]ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. ๐Ÿ–Š

Ni ahadi ambayo Bwana Yesu aliitoa kwa wanafunzi wake, kabla ya kupaa na kwenda mbinguni baada tu ya kufufuka kwake, aliwaahidi wanafunzi wake akisema sitawaacha ninyi yatima bali nitawafanyia msaidizi, kwa maana Yesu alijua hakuna namna mwanadamu anaweza akajitegemea yeye mwenyewe binafsi, kwa sababu ya udhaifu tulio nao, hivyo tunakamilishwa na Kristo Yesu, hata maandiko yanasema katika
kitabu cha;

Yeremia 17:5-8
[5]BWANA asema hivi,
Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu,
Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake
Na moyoni mwake amemwacha BWANA.

[6]Maana atakuwa k**a fukara nyikani,
Hataona yatakapotokea mema;
Bali atakaa jangwani palipo ukame,
Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

BALI;

[7]Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA,
Ambaye BWANA ni tumaini lake.
[8]Maana atakuwa k**a mti uliopandwa kando ya maji,
Uenezao mizizi yake karibu na mto;
Hautaona hofu wakati wa hari ujapo,
Bali jani lake litakuwa bichi;
Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua,
Wala hautaacha kuzaa matunda. ๐Ÿ–Š

KUTEMBEA NA ROHO MTAKATIFU.

Jifunze sana kutembea na Roho Mtakatifu mpendwa utafurahia sana.....

Mtu anayetembea na Roho wa Mungu hakuna namna atashindwa katika maisha, labla awe nje ya uongozi wa Roho wa Mungu, tunaishi maisha ya kawaida sana kwa sababu hatutaki kuongozwa na Roho wa Mungu.

Ukiwa unatembea na Roho Mtakatifu utaishi kwa kujiamini na unakuwa na uhakika wa maisha ya hapa duniani ya yajayo..

(Your life is guaranteed once you're walking with the Holy spirit / Holy Ghost)

Hapa tutajifunza namna ambayo Roho Mtakatifu anaweza kujifunua au kujidhirisha kwa mtu katika maeneo matatu na faida ya matokeo yake.....

i) Eneo la kwanza, Roho Mtakatifu anapokuwa juu yako, Roho Mtakatifu anapokuwa juu yako matokeo yake ni kwamba anakupa nguvu za kiroho, hebu tutazame katika kitabu cha;

Matendo ya Mitume 1:8
[8]Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
Pia kitabu cha;

Luka 1:35
[35]Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika k**a kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.

Ufafanuzi;
Hii ni kwa habari ya Mariamu wakati ule anapashwa habari njema na Malaika wa Bwana ya kwamba atachukua mimba na kumzaa Yesu, alipomuuliza litakuwaje neno hili ndipo akamjibu kuwa, Roho wa Mungu atakujilia juu yako, na nguvu za aliye juu zitakufunika k**a kivuli.....๐Ÿ–Š

Pia ukisoma kitabu cha Waamuzi, kinaeleza kwa namna Roho ya Bwana ilivyomjilia Samsoni kwa nguvu, hajasema ilimjilia wapi? Lakini uwe na uhakika ilimjilia juu kwa nguvu ndipo akaweza kumpasua yule mwana - simba kana kwamba anampasua
mwana - mbuzi, hadithi hii nzuri na ya kusisimua inayoelezea ukuu wa Mungu inapatikana katika
kitabu cha;........

Waamuzi 14:5-6
[5]Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia.

[6]Roho ya BWANA ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.

Lakini pia, Roho Mtakatifu akikujilia juu yako si tu utapokea nguvu za kiroho, bali pamoja na karama za Rohoni k**a vile kunena kwa lugha au kusema kwa lugha mpya pamoja na kutabiri, tuangalie kwa pamoja kitabu cha;

Matendo ya Mitume 19:6
[6]Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri...๐Ÿ–Š

ANGALIZO;
Kuwa na karama za Roho Mtakatifu, haimaanishi uko na Roho Mtakatifu ndani yako, zingatia hili inawezekana haujanielewa, yaani ukiwa na karama ya kunena kwa lugha au kutabiri au upako wa Mungu, sio kigezo kwamba wewe una Roho Mtakatifu, kwa sababu hizo ni karama za Roho Mtakatifu lakini sio yeye,

Kuna mtu anajiuliza swali sasa nawezaje kunena kwa lugha au kutabiri bila Roho Mtakatifu? Ndio inawezekana kwa sababu ile ni karama umepewa, unaweza kuitumia hata bila ya Roho Mtakatifu, ingawaje inakuwa bora sana, ukiwa na hiyo karama pamoja na Roho Mtakatifu hapo ndipo utakapoona maajabu ya Mungu.

Kwahiyo usiupime wokovu kwa karama zinazofanya kazi ndani yako, bali jipime kwa matendo yako k**a unaishi maisha matakatifu, nadhani hicho ndio kipimo bora, wewe unafikiri kwa nini Yesu anasema sio kila anayelitaja jina la Bwana ataurithi ufalme wa Mungu, hebu tazama katika kitabu cha;

Mathayo 7:21,23
[21]Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Hapa anazungumzia wale wanaojiongoza kwa hekima ya kibinadamu na wamemuacha Bwana na ndio hao Yesu anawazungumzia ya kuwa siku ya mwisho ya hukumu, wengine watasema Bwana tazama mimi nilihubiri sana neno lako, nilitoa pepo kwa jina lako, nilitabiri kwa jina lako, lakini Bwana Mungu atawaambia siwajui ninyi, tazama katika kitabu cha;

Mathayo 7:22-23
[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.

Watu wengi sana wa kizazi hiki (cha uasi) hawamuhitaji Roho Mtakatifu na wala hawana mpango wa kutembea na Roho Mtakatifu bali wanahitaji nguvu zake tu ili ziwasaidie katika mambo yao, ndio maana tumekuwa na watu wanaotafuta miujiza tu! Sina maana ni vibaya lakini nia yako ni nini!, na Bwana Mungu anatazama nia ya ndani ya mtu wala Mungu hawezi kuhukumu matendo bali nia ya mtu maana matendo ya mtu ni matokeo ya kile alichokifanya tayari katika moyo wake, sikiliza mpendwa kutembea na Roho Mtakatifu ni gharama na unatakiwa ujikane kabisa, maana Yesu anasema wazi ya kuwa atakaye kunifuata na ajikane mwenyewe na ajitwike msalaba na anifuate katika kitabu cha;

Mathayo 16:24-26
[24]Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

[25]Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

[26]Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

ii) Eneo la pili, Roho Mtakatifu anapokuwa ndani yako, Roho Mtakatifu anapokuwa ndani yako ina maana kuwa anakuongoza katika njia itakayompendeza Bwana Mungu,

Yohana 14:17
[17]ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Yohana 16:13
[13]Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Mpendwa katika Bwana chagua leo kuongozwa na Roho wa Mungu, kwani maisha yako yatakuwa yenye kusisimua na yenye furaha ya kudumu, kwa maana hata maandiko ya Mungu yanasema kuwa wanaoongozwa na Roho hao ndio wana wa Mungu, tutazame kwa pamoja kitabu cha;

Warumi 8:14
[14]Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.

Watu wanaoongozwa na Roho utawatambua kwa matunda yao, kwa sababu ikiwa unaongozwa na Roho Mtakatifu watu wataona matokeo ya tunda la Roho.

DALILI AU MATOKEO ZA/YA MTU ANAYETEMBEA NA ROHO MTAKATIFU..

Dalili au matokeo ya mtu anyeongozwa na Roho Mtakatifu, msingi wake umetoka katika kitabu cha Wagalatia.........

Mathayo 7:16-18
[16]Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?

[17]Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.

[18]Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.

Wagalatia 5:22-23
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

[23]upole, kiasi; juu ya mambo k**a hayo hakuna sheria.

a) Upendo, hii ni amri kuu tuliyopewa wakristo, hivyo kila mkristo wa kweli na mwenye kumpenda Mungu yafaa awe na upendo kwa wengine, kwa sababu Mungu ni pendo, 1 Yohana 4:16
[16]Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.

1 Wakorintho 13:1-3
[1]Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, k**a sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

[2]Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, k**a sina upendo, si kitu mimi.

[3]Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, k**a sina upendo, hainifaidii kitu.

Mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu atakuwa na upendo wa Agape, yaani pendo la Kristo, huu ni aina ya upendo ambao hautarajii vitu, ndipo umpende mtu, (unconditional love) upendo huu hauna unafiki bali ni wa kweli,

Warumi 12:9-10
[9]Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.

[10]Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;

Hivyo asiye na upendo hakumjua Mungu, sawa sawa na kitabu cha;

1 Yohana 4:8,16
[8]Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.

Na ikiwa unampenda mtu kwa sababu yeye anakupenda pia, hakuna upendo wa kweli, kwa sisi wakristo ni kuwapenda hata wale wanatuudhi,

Mathayo 5:43-44
[43]Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

[44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Kwa kufanya hivyo utakuwa unawavuta watu kwa Kristo..

Lakini watu leo hii upendo umepungua, k**a yasemavyo maandiko ya kuwa upendo wa wengi utapoa, Mathayo 24:12
[12]Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.

Ukijitathimini na kujiona uko na dalili hii sio tu siku za mwisho bali pia hauna Roho Mtakatifu......๐Ÿ–Š

b) Furaha, hii pia ni dalili nyingine ya kuwa unaongozwa na Roho Mtakatifu, ni kuwa na furaha, na ikiwa wewe ni mtu wa kununa tu au furaha yako inategemea kukamilishwa na vitu kwa maana ya fedha mali nk.

Basi ni dhahiri kuwa hauna Roho Mtakatifu, kwani furaha yetu haitegemei vitu au mali, bali furaha yetu inategemea kukamilishwa na Pendo la kristo Yesu, kitabu cha Wafilipi kinathibitisha hilo.........

Wafilipi 4:4
[4]Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.

USHUHUDA;
Kuna rafiki yangu mmoja tulikuwa tukiomba pamoja, na tuliomba, Mungu atujarie furaha na amani ya Kristo itawale kwa siku hiyo, hakika Bwana Mungu ni wa ajabu sana, nakumbuka alinitumia ujumbe kwa njia ya simu jioni, "My friend by ths happiness you can be crazy. Watu wanaweza wasikuelew kbxa.Mungu ni wa ajabu sana" alisema huyo rafiki yangu, hii inanipa nguvu kuwa haijarishi uko na hali gani lakini ukiwa na Roho Mtakatifu ndani yako, unaiona dunia k**a yote ni yako.......๐Ÿ–Š

c) Amani, hii ni dalili nyingine ambayo inadhihirisha ya kuwa unaye Roho Mtakatifu au hauna, ikiwa una amani si kwa sababu ya vitu au mali au pengine maisha kukuendea vizuri, basi ni dhahiri unaongozwa na Roho Mtakatifu, k**a vile yasemavyo maandiko ya kuwa amani niwapayo mimi si k**a ulimwengu uwapavyo....

Yohana 14:27
[27]Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo k**a ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.

Hivyo, jitathimini mpendwa ikiwa amani uliyonayo ni kwa sababu ya hali nzuri ya kimaisha, na pindi mambo yakikuendea mlama unakosa amani na pengine unachukia kila mtu kwa shida yako mwenyewe, ukiona hivyo jua kabisa hauna uongozi wa Roho Mtakatifu...๐Ÿ–Š

d) Uvumilivu, mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu amejifunza kuwa mvumilivu, na ujue kabisa tunapozungumzia uvumilivu, ieleweke kuwa uvumilivu katika mambo magumu na mazito, inawezekana watu wanakusema vibaya na umejua, swali ni je? Unaweza kuvumilia au kunyamaza! Au umeoa au umeolewa na hamjapata mtoto na kwa muda sasa, je! Unaweza kuvumilia, nadhani hiki ni kipimo bora cha kuwa wewe unaongozwa Roho Mtakatifu la!......

Ikiwa Roho Mtakatifu anakuongoza lazima atakufundisha kuvumilia hali yoyote ile, bila kumtupia mtu lawama katika mambo unayoyapitia..

Warumi 5:3-5
[3]Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;

[4]na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;

[5]na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.

Ufafanuzi;
Kwahiyo mtume Paulo anasema kuwa wala si hivyo tu! bali tufurahi katika dhiki pia, maana dhiki kazi yake ni kuleta saburi yaani uwezo wa kuvumilia na kuhimili mambo, na kazi ya saburi ni kukupa uthabiti wa moyo, na kazi ya uthabiti wa moyo ni kukupa tumaini, maana yake kuwa na uhakika na matarajio na tumaini halitayarishi yaani haliaibishi kwa sababu tunajua ya kuwa Yesu anatupenda..

Lakini pia katika kitabu cha Wafilipi kinaendele kuelezea juu ya kufunzwa kuvumilia..

Wafilipi 4:11-13
[11]Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.
[12]Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.
[13]Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu......๐Ÿ–Š

e) Utu wema, hii ni dalili nyingine inayodhihirisha ikiwa una Roho Mtakatifu au la, na itakupa majibu ikiwa unaongozwa na Roho Mtakatifu au la!, utu wema ni pamoja na kujari wengine na kuwasaidia kwa nafasi yako bila kujari ni nani, kwahiyo ili uwe na utu wema na wa kweli lazima uwe na Roho Mtakatifu..

Haujawahi kuona mahali watu wanafurahia mwingine anapopata shida, hiyo siyo Roho ya Mungu , bila shaka unakumbuka kisa cha Yesu na wanafunzi wake pale ambapo wale wenyeji hawakumkaribisha Yesu, basi wanafunzi wake Yesu Yohana na Yakobo wakamwambia Yesu, Bwana unataka tuagize moto uwaangamize k**a alivyofanya Eliya, ndipo Yesu akawajibu akawaambia hamjui roho iliyoko ndani yenu ni ya namna gani, tazama kitabu cha;

Luka 9:54-55
[54]Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [k**a Eliya naye alivyofanya]?

[55]Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] ,, ,, ๐Ÿ–Š

f) Fadhili, hii ni dalili nyingine inayodhirisha ya kuwa una Roho Mtatifu, utakuwa ni mtu mwenye kufadhili wengine ambao yamkini hawajiwezi kiuchumi na kuwasaidia yatima, wajane na wengine wenye mahitaji, kwa kufanya hivyo inadhihirisha ya unaye Roho Mtakatifu ambaye anakuhimiza kuyafanya hayo.

Ila k**a hauna Roho Mtakatifu ni ngumu sana kufanya hivyo, kusaidia wengine kwa maana kwako ni hasara unaona k**a unatupa pesa lakini ukienda baa unatumia pesa ovyo bila hata kujari lakini linapokuja suala la kusaidia watu wenye mahitaji unaona bajeti yako inagoma, ni dalili tosha ya kuwa hauna Roho Mtakatifu, bila shaka unamkumbuka Kornelio Akida wa Jeshi Biblia inaniambia alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, sasa watu wengine wanafikiri sadaka ni ile tu unatoa kanisani, lakini wakimpa mtu asiyejiweza wanaona wametoa msaada, hebu tutazame kitabu cha;

Matendo ya Mitume 10:1-2
[1]Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,

[2]mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.......๐Ÿ–Š

g) Uaminifu, uaminifu ni dalili moja wapo ikiwa una Roho Mtakatifu, wakati mwingine watu wanafanya mambo kwa kujificha, lakini ukweli ni kwamba unafanya hivyo kwa sababu hauna Roho Mtakatifu.

Kuna watu wameokoka kabisa lakini sio waaminifu wakipewa kazi wanaiba yaani hakuna tofauti kati ya aliyeookoka na ambaye hajaokoa maana wanakwenda sambamba, sikiliza mpendwa tunafaa kuwa kielelezo bora cha Kristo Yesu ili na wengine kwa matendo na mwiyenendo yetu wavutwe kwa Yesu, Tito anatukumbusha tuwe waaminifu tusiwe waibaji, katika kitabu cha Tito.

Tito 2:10
[10]wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.

Kwa nini usimuwakilishe vyema huyo Yesu unayemtaja na hata watu wakikuona basi wajue ya kuwa unaye Yesu.....๐Ÿ–Š

h) Upole, hii pia ni dalili ya kuwa unaye Roho Mtakatifu, sasa nifafanue kidogo maana ya upole maana watu wengi wanachanganya, mtu mpole haimaanishi mtu ambaye sio muongeaji au mkimya, mara nyingi watu wanafikiri mtu mpole ni yule ambaye mkimya, hapana.

Mtu mpole ni mtu asiye na makuu, hata utakapomfanyia jambo baya atakuonya kistaarabu na pasipo kutaka uaibike...

2 Timotheo 2:25
[25]akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili k**a ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

Wafilipi 4:5
[5]Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu.

Sasa ikiwa una dalili hii basi ujue wewe unaye Roho Mtakatifu, kwetu sisi wakristo hatuna jino kwa jino....๐Ÿ–Š

i) Kiasi, hii dalili ya mtu mwenye Roho Mtakatifu lazima kuwa na kiasi katika mambo yote, ukiwa na kiasi mambo hayakinai..๐Ÿ–Š

1 Petro 5:8
[8]Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa msh*taki wenu Ibilisi, k**a simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

Bwana Yesu asifiwe sana mpendwa mtu wa Mungu hongera sana kwa kuendelea kufuatilia masomo haya hautabaki k**a ulivyo na ni maombi yangu Mungu wa Mbinguni akujarie maarifa ya kimungu zaidi na zaidi.

iii) Eneo la tatu, Roho Mtakatifu anapokuwa pamoja na wewe maana yake, ni ushirika na wewe, tazama katika kitabu cha;

2 Wakorintho 13:14
[14]Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Na kati ya kitu Roho Mtakatifu anapenda ni ushirika na sisi wanadamu, na ushirika na Roho Mtakatifu una maana ya kukushirikisha mambo mbalimbali yanayokuhusu wewe na watu wengine pia, kuna wakati unaweza ukamshirikisha Roho Mtakatifu kila kitu hata kuhusu kula kwako kuvaa marafiki na mengine mengi kwa nini kwa sababu Roho Mtakatifu anajari sana juu ya maisha yetu naye hujishughulisha sana na mambo yetu, sawa sawa na kitabu cha;

1 Petro 5:7
[7]huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.

Wafilipi 2:1-2
[1]Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema,

[2]ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja.

Tamani kushirikishana na Roho Mtakatifu, utaona mtembeo mpya wa kimungu katika maisha yako, mwambie chochote na kuna wakati ukiwa na ushirika mzuri na Roho Mtakatifu kuna vitu ukiviwaza tu na kuvitamani ghafla unashanga amekupatia kwa namna ya ajabu mpaka utashangaa, binafsi nafurahia sana ushirika na Roho Mtakatifu. ....๐Ÿ–Š

Bwana Mungu alibariki Neno lake akubariki na wewe uliyesoma.....

Omba kwa ajiri ya Tanzania, usinyamaze mpendwa.,๐Ÿ‡น๐Ÿ‡ฟ

Endelea kufuatilia maarifa haya ya kimungu siku kwa siku na utajikuta umekuwa haraka kihoho....

Bwana Mungu akubariki na kukulinda na akuangazie nuru za uso wake na kukufadhili katika maisha yako......

Endelea kumpenda Yesu.

Makala hii ya Roho Mtakatifu imeandaliwa na,

Mwl. Chusi Steven.
+255742874709
05/05/2023
Arusha - Tanzania

Address

Mkwawa
Iringa
CHUSI1444

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when MWL. CHUSI posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share

Category