11/08/2026
Baba na mtoto wake wamenusurika kifo baada ya baba huyo kumtumbukiza mtoto kisimani, kisha naye kujirusha ndani ya kisima hicho, huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa ni
mgogoro wa kifamilia kati yake na mke wake.
Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Kasimba, ambapo mashuhuda wamesema baba huyo alitoka ndani ya nyumba akiwa na mtoto wake huku akikimbia na kusema, “Bora afe yeye na mtoto wake.”
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kasimba, Leonard Nswima, amesema alipigiwa simu na majirani na kupewa taarifa kuhusu baba na mtoto hao kutumbukia kisimani.
Kelvin Ponela, mtaalamu kutoka Kituo cha Afya Ilembo, amethibitisha kuwapokea majeruhi hao na kusema kuwa hali zao zinaendelea vizuri.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limetoa rai kwa wananchi kuwa na desturi ya kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya amani, kwa kuwashirikisha ndugu, viongozi wa dini au viongozi wa serikali, jambo ambalo litasaidia kuzuia vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.